Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Senegal Aliou Cisse, amewaomba radhi Mashabiki wa Soka nchini humo, kufuatia kikosi chake kushindwa kutetea Ubingwa wa AFCON 2023, kwa kuondolewa na wenyeji Ivory Coast juzi Jumatatu (Januari 29).
Senegal ‘Simba wa Teranga’ waliondoshwa katika Fainali za ‘AFCON 2023’ kwa kufungwa kwa mikwaju ya Panati 5-4, baada ya mchezo huo wa Hatua ya 16 Bora kumalizika kwa sare ya 1-1 katika muda wa kawaida.
Miamba hiyo ya Afrika ya Magharibi ilitangulia kupata bao la mapema katika dakika ya nne kwa bao la Habib Diallo huku Sadio Mane akitoa pasi ya bao.
Wenyeji ‘The Elephants’ walisawazisha dakika ya 86 na Franck Kessie akifunga kwa mkwaju wa Panati, ambao ulilazimika kwenda kuchunguzwa kwa VAR.
Kocha Cisse amesema kuondolewa kwao ni kimekuwa kama pigo kubwa sana kwao, lakini hawana budi kukubaliana na matokeo ya mchezo wa Soka, ambayo wakati mwingine huwa katili kwa timu bora.
“Nimesikitishwa baada ya matokeo haya, haswa kwa wachezaji wetu. Tulikuja hapa kushinda taji na kuwafurahisha mashabiki wetu. Hayo ndio matokeo ya mchezo wa soka, mwaka 2022 tulifurahi, na 2024 imekuwa kinyume chake.” amesema Cisse
“Ninawapa pole kwa wachezaji wangu wote. Ni vigumu kuona wachezaji wakilia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.”
“Mechi ilikuwa ya ajabu na ngumu, tungeweza kushinda mchezo. Tulipoteza kwa mikwaju ya Penati, tuliendelea kuongoza hadi dakika 5 za mwisho za mechi.”
“Nimesikitishwa baada ya kushindwa huku, haswa baada ya mchezo tuliocheza wakati wa mechi na mechi ya kwanza ya mashindano.
“Tunahitaji kufanya mabadiliko baada ya kushindwa huku, tutaona kitakachotokea siku zijazo. Kuna huzuni, na wachezaji wetu wana huzuni, kama ilivyo kwa watu wa Senegal.
“Tulijiandaa vyema kwa mashindano haya, na tusisahau tumeshinda mara tatu katika mechi tatu za hatua ya makundi,” amesema Cisse