Wadau wa sekta mipango miji, wamekutana Jijini Dodoma kujadili rasimu ya marekebisho ya Kanuni za Sheria za Mipango Miji nchini ili ziendane na mabadiliko ya kasi ya ukuaji miji pamoja mchango wake wa sekta hiyo katika hafua muhimu za kuifadhi mazingira.
Akifungua kikao hicho jijini Dodoma, Naibu Katibu Wizara ya ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Lucy Kabyemera amesema kuwa ardhi inahitaji kupangwa, kupimwa, kumilikishwa na kuendelezwa ikiwa katika hali nzuri kiuchumi, kijamii na kimazingira.
Amesema, “natambua ili kufanikisha azma hii, tunahitaji kuwa na kanuni sahihi za kuongoza upangaji wa miji yetu pamoja na matumizi mbalimbali ya ardhi hapa nchini.”
Upangaji miji, unaongozwa na Sheria ya Mipango Miji sura Na. 355 na Kanuni zake za mwaka 2018 ambazo zinahitaji kuboreshwa kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, kimazingira, mitazamo ya kimaisha, kimaendeleo pamoja na mitazamo ya kimataifa vimekuwa msingi wa kupitia upya kanuni hizo ili ziendane na hali ya sasa.
Wadau hao ni pamoja na Manejimenti ya Wizara, Makamishna wa Ardhi Wasaidizi kutoka mikoa ya Tanzania Bara, wawakilishi kutoka Wizara mbalimbali, taasisi za Serikali pamoja na zisizo za Serikali.