Mkuu wa Wilaya Mbeya, Beno Malisa amewataka walimu kwa kushirikiana na Viongozi Kata kufanya zoezi la kubaini Wanafunzi waliohamishiwa shule binafsi na wale ambao hawaendi shule na wapo nyumbani ili kuchukua hatua kwa Wazazi watakaobainika kuwa sababu kutoripoti shule.
Akitoa agizo hilo, Malisa amesema idadi ya Wanafunzi walioripoti inafikia asilimia 91 kwa Wilaya ya Mbeya hivyo ni vyema hatua zikachukuliwa kubaini wale wachache wasioripoti shule wanakabiliwa na changamoto zipi, ili kufikia asilimia 100.
Awali, katika ripoti iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mbeya, Stephene Katemba amesema kuhamishiwa kwa baadhi ya wanafunzi katika shule binafsi kumepunguza idadi ya wanafunzi waliotakiwa kiripoti katika shule walizopangiwa.
Akiwa katika kata ya Nsalala, Malisa ametembelea Shule ya Sekondari ya Nsalala kukagua mahudhurio ya Wanafunzi wa Kidato cha kwanza, kuzungumza na Wanafunzi kisha kutembelea na kukagua bweni linalojengwa kwa ajili ya Wanafunzi wenye mahitaji maalumu.