Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dkt. Festo Dugange amesema katika miaka mitatu Serikali imeajiri watumishi wa kada ya afya 18,418 na kutumia shilingi 195.3 bilioni kujenga miundombinu ya Hospitali za Wilaya 136 na ukarabati wa Hospitali kongwe 19.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii jijini Dar es Salaam, Dugange amesema serikali pia imejenga vituo vya afya 446 kwa sh.bilioni 718.18, ujenzi wa zahanati 955 kwa gharama ya Sh.bilioni 77. 41, majengo ya dharura 80, wagonjwa mahututi 28 na nyumba za watumishi 150 kwa gharama ya sh. bilioni 45 ili kuboresha huduma za afya na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kuhusu wahudumu wa ngazi ya jamii, amesema ni watu muhimu ndani ya jamii kwa kuwa wao ndio daraja kati ya jamii na vituo vinavyotoa huduma za afya nchini ili wananchi wawe na afya njema na kuongeza kuwa, “kupitia mpango jumuishi wa wahudumu wa afya ya jamii weledi na maarifa ya wahudumu hawa utaongezeka sambamba na wigo wa huduma wanazozitoa.”
Aidha, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi ndio itakuwa na jukumu la kusimamia zoezi la kuwapata wahudumu wa afya ngazi ya jamii watakaojumuishwa kwenye mpango huo na tayari imeandaa taratibu na vigezo vya kuwapata wahudumu hao na mchakato wake utakuwa wa wazi ili kuwapata wanajamii wenye sifa na vigezo vinavyotakiwa.