Beki wa Kulia wa Timu ya Taifa ya Morocco ‘Simba wa Milima ya Atlas’ Achraf Hakimi ameomba radhi kwa kukosa Penati ambayo huenda ingewapa nguvu wachezaji wenzake katika mchezo wa Hatua ya 16 Bora dhidi ya Afrika Kusini Juzi Jumanne (Januari 30).
Morocco ilikua nyuma kwa bao moja dhidi ya Afrika Kusini na ilipata mkwaju huo dakika ya 84, huku ikiwa nyuma kwa bao moja lakini Hakimi hakufanikiwa kuukwamisha mpira wavuni.
Beki huyo aneyewatumikia Mabingwa wa Soka nchini Ufaransa PSG, imemchukuwa muda kuomba radhi kwa kitendo hicho, ambacho kiliongeza morari kwa Afrika Kusini kupata bao la pili na la ushindi.
“Ilikuwa siku ngumu sana na ya huzuni kwa kuondolewa kwenye michuano ya AFCON 2023,”
“Ninaomba radhi kwa kilichotokea, Nilichukua jukumu la kuisaidia timu yangu na Taifa langu, lakini kwa bahati mbaya, sikufanikiwa kufikia lengo ambalo lingeturudisha mchezoni.”
“Nataka kuwashukuru watu wote wa Morocco kwa msaada wao, hasa watu wote waliokuja Ivory Coast. Tutasimama na kurudi kwa nguvu zaidi kuanzia sasa! Mungu akipenda.” Hakimi ameandika kwenye Instagram.
Hakimi pia ametuma ujumbe wa kumuunga mkono winga wa Morocco, Amine Adli, ambaye kwa huzuni alimpoteza kaka yake kabla ya mchuano hiyo.
“Baada ya yote uliyopitia, ulikuja na kutoa yote kwa ajili ya nchi yako. Tunajivunia wewe! Nakupenda sana kaka,” ameandika.
Licha ya uchungu wa kushindwa na Afrika Kusini, Hakimi alionyesha ari yake ya kucheza kwa kwa kujituma, huku akiwatakia Bafana Bafana mafanikio mema katika michezo iliyosalia.