Uongozi wa Klabu ya Simba SC umeziita mezani Klabu za AS Far Rabati ya Morocco na Al Ahly ya Misri, zinazotajwa kuhitaji huduma ya Beki kutoka DR Congo Henock Inonga.
Tetesi za Inonga kutakiwa na klabu hizo zilizagaa baada ya mchezaji huyo kufanya vizuri katika Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zinazoendelea nchini Ivory Coast.
Inonga yupo kwenye Fainali za ‘AFCON 2023’ akiwa na timu yake ya Taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), ambayo inajiandaa kucheza mechi ya Robo Fainali.
Katika michuano hiyo, Inonga amecheza michezo yote mitatu ya hatua ya makundi dhidi ya Tanzania, Morocco na Zambia, pia dhidi ya Misri katika hatua ya 16 bora na alionesha kiwango kizuri kilichowavutia vigogo hao wa Afrika.
Akizungumza kwa njia ya mtandao, nyota huyo amesikia tetesi za kutakiwa na klabu hiyo lakini hakuna kiongozi yoyote aliyewasiliana naye.
“Mimi bado nina mkataba na Simba SC, siwezi kuzungumzia kuondoka wala kubaki wanaoweza kuwa na majibu sahihi ni waajiri wangu,” amesema nyota huyo.
Meneja wa Habari na Mawasilino Simba SC, Ahmed Ally amesema hawajapokea taarifa kutoka klabu yoyote ambayo inamuhitaji mchezaji huyo.
“Hadi sasa hakuna ofa iliyofika mezani juu ya Inonga, hata sisi tunaona hizi taarifa za kutajwa FAR Rabat na Al Ahly katika mitandao.”
Achraf Hakimi awaomba radhi Mashabiki
“Kama kuna ofa kubwa hakuna kinachoshindikana, waje tuzungumze na kukubaliana, mambo yakiwa sawa hakuna kinachoshindikana,” amesema Ahmed.
Simba SC ambayo jana Jumatano (Januari 31) ilishuka dimbani katika mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam ‘ASFC’, inajiandaa na michezo ya viporo ya Ligi Kuu dhidi ya Mashujaa FC, Tabora United na Azam FC.