Pichani ni eneo la Makoko, ni makazi yasiyo rasmi yaliyopo eneo la Daraja la 3 bara, lililoko Pwani ya Lagos Nchini Nigeria. Theluthi moja ya makazi ya jamii ya watu wa hapa imejengwa juu ya nguzo Ziwani na iliyobaki iko kwenye ardhi.
Zoezi la upangaji miji halikuzingatiwa mahala hapa na licha ya uwepo wa maji lakini jamii ya eneo hili haikujali, walitafuta kila mbinu kuhakikisha wanaishi juu ya maji, ili kuwa jirani na Samaki.
Sehemu ya mbele ya eneo hili, inamilikiwa na watu wa Egun ambao walihamia hapo wakitoka Badagary, Togo na Jamhuri ya Benin wakifuata mkate wao wa kila siku, kwa kazi yao kuu ambayo ni uvuvi.
Makoko wakati mwingine inajulikana kama “Venice ya Afrika” na hii ni kutokana na njia zake za maji huku idadi ya wakazi wake ikihisiwa kufikia watu 85,840.
Hata hivyo, eneo hilo halikuhesabiwa rasmi kama sehemu ya sensa ya watu na Makazi mwaka 2007, licha ya idadi kubwa ya watu kuzidi kuongezeka kwa kuzaliana na uhamiaji.
Julai 2012, Serikali ya Jimbo la Lagos chini ya Gavana Babatunde Fashola iliamuru nguzo kwenye kingo za maji za Iwaya/Makoko zibomolewe ndani ya saa 72 za notisi kwa wakazi wa eneo hilo, ambapo takriban watu 3,000 walipoteza nyumba zao na kuwafanya waishi kwa hofu ya kuporwa kwa eneo lao.
Miezi miwili baada ya kubomolewa kwa sehemu hiyo, Shirika la Serac Urban Spaces Innovation liliandaa mpango wa uundaji upya wa Makoko, ambao ungeileta jamii hiyo pamoja na wasomi, mashirika yasiyo ya faida na washauri wa kimataifa.
Mpango huo, uliwasilishwa kwa Wizara ya Mipango ya Miji na Kimwili ya Jimbo la Lagos mnamo Januari 2014 baada ya kugundua hila za Serikali kutaka kurasimisha eneo hilo kimabavu, ili kuweka mikakati upya ya upangaji wa makazi ambao ulishitukiwa mapema.
Bila shaka Wataalamu wetu wa mipango miji hawatakiwi kusubiri mambo kama haya, kwa kushirikiana na Serikali ipo haja ya kuandaa mipango ya kitaifa itakayowezesha utu wa makazi kwa watu wake na hivyo kuondokana na athari za kiafya kwa magonjwa ya milipuko na na zile za kiuchumi.