Nahodha wa Black Stars, Andre Ayew amewaomba radhi Mashabiki wa Soka nchini Ghana baada ya timu ya taifa ya soka ya nchi hiyo kuboronga kwenye Fainali za ‘AFCON 2023’ na kutupwa nje kwenye hatua ya makundi.
Ayew alirekodi video akiwaambia Wananchi wa Ghana kwamba watarudi kwenye Fainali nyingine wakiwa wenye nguvu na kwamba wachezaji wote wa timu hiyo wanafahamu hasira walizo nazo Mashabiki wao.
Wanamuziki wa Afrika, Davido na Sarkodie walikuwa miongoni mwa watu waliokomenti kwenye video hiyo ya Ayew ya kuomba radhi kwa Mashabiki.
Ayew amesema siku chache zilizopita Mashabiki wa Ghana wamekuwa kwenye wakati mgumu kutokana na matokeo yasiyoridhisha yaliyovunwa na kikosi chao kwenye fainali hizo zilizofikia hatua ya Robo Fainali huko Ivory Coast.
Kwenye video, Ayew alisema: “Napenda kuomba radhi kwa matokeo tuliyoyapata na kutupwa nje. Tunafahamu tulipaswa kufanya vizurii. Hilo lingefanyika tungepata matokeo mazuri kama taifa.”
Nahodha huyo wa Black Stars aliongeza: “Kwenye soka vitu kama hivi vinatokea, vitu kama hivi vinakufanya kuwa na nguvu. Na kisichokuua, kitakupa ukomavu kama mmoja mmoja au kundi.”
Kutokana maneno hayo ya Ayew, Davido alikomenti: Hakuna kilichoharibika baba!!