Klabu ya Prisons imeanza kupima afya wachezaji wake kabla ya kuingia kambini kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans itakayochezwa Februari 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Sokoine, Mbeya.

Ofisa Habari wa Prisons, Issaka Chacha, amesema kikosi hicho tayari kimeshaanza mazoezi ya utimamu wa mwili, lakini kabla hawajaanza kufanya hivyo wachezaji wote walipimwa afya ili kuangaliwa kama wanaweza kuhimili aina hiyo ya mazoezi magumu, lakini kuanza maandalizi ya mechi za lala salama.

“Unajua ligi imesimama kwa muda sasa kupisha Kombe la Mapinduzi na AFCON 2023, sasa waliporudi wachezaji wetu wote waliingia kwenye vipimo, na sisi hatutanii tunapima kweli, sisi ni maafande,” amesema Ofisa Habari huyo mpya ambaye amechukua nafasi ya Jackson Mafulango.

Alizitaja sababu za kuwapima afya wachezaji ambao tayari wamesajiliwa tofauti na klabu zingine ambazo huwapima wakati wa usajili.

“Tumepima afya za wachezaji, kwa sababu walikuwa mapumziko, kwanza tulitaka kujiridhishe je, wanaweza kuanza mazoezi ya nguvu?

Kwa sababu ligi ilisimama na walikuwa mapumziko, haiwezekani kuwafanyisha mazoezi makali bila kuwapima. Nia ni kujiweka tayari na michezo yetu ya Ligi Kuu, tukianza na Young Africans,” amesema.

Ameongeza licha ya kuondokewa na Edwin Balua aliyejiunga na Simba SC, wamefanya usajili wa wachezaji watano ambao wanaamini watakiongezea nguvu kikosi chao.

Walioiba Majeneza Msikitini kusomewa kisomo
Pep Guardiola kufuata nyayo za Klopp