Baada ya matokeo ya kushangaza tangu kuanza kwa mashindano ya 34 ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ yanayoendelea nchini Ivory Coast, Nigeria ‘Super Eagles’ leo Ijumaa (Februari 02) wanashuka dimbani kucheza dhidi ya Angola katika mchezo wa Robo Fainali.
Nigeria ambao ni mabingwa mara tatu wa AFCON wanakutana na Angola katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Felix Houphouët-Boigny mjini Abidjan kuanzia saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.
Hatua hiyo ya Robo Fainali inazikutanisha jumla ya nchi nane huku tayari baadhi ya vigogo wakiwa nje na kuziacha timu ambazo hazikupewa kabisa nafasi hata ya kucheza hatua ya 16, lakini sasa ziko Robo Fainali.
Nchi zote nane zinazoshiriki Robo Fainali katika mashindano ya 34 ambayo ndio mashindano makubwa zaidi ya soka Barani Afrika zinaweza kupata matokeo ambayo ama yatakuwa kicheko au maajabu.
Katika mchezo mwingine wa Robo Fainali leo kuanzia saa 5:00 usiku, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) watatoana jasho na Guinea.
Mohamed Bayo amekuwa mkombozi mara mbili kwa Guinea katika michuano ya AFCON 2023.
Alifunga dhidi ya Cameroon na kuwasaidia kupata pointi na alikuwa kwenye kikosi kilichocheza dhidi ya Guinea ya Ikweta katika raundi ya 16.