Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anadaiwa kukubali yaishe kwenye ishu ya straika na amepanga kusubiri hadi mwisho wa msimu kabla ya kuingia tena kwenye mazungumzo ya kusajili mashine kwenye eneo hilo.
Arteta alikuwa akihitaji kuboresha eneo la ushambuliaji na miongoni mwa mastraika ambao walikuwa kwenye rada zake ni Ivan Toney na Victor Osimhen.
Hata hivyo, chaguo la kwanza ilikuwa ni Toney, lakini staa huyo ambaye mkataba wake unamalizika mwaka 2025, anadaiwa kuwajibu kwamba anataka kusalia Brentford hadi mwisho wa msimu.
Kwa upande wa Osimhen kiasi cha pesa kilichohitajika kilionekana kuwa ni kikubwa tofauti na bajeti ya Arsenal, vilevile SSC Napoli haikuonekana kuwa tayari kutaka kumruhusu hadi mwisho wa msimu.
Mpango wa kusajili Mshambuliaji ulikuwa ni kwa sababu ya majeraha ya mara kwa mara ambayo Gabriel Jesus amekuwa akiyapata hali inayosababisa muda mwingi kuwa na Eddie Nketiah pekee yake.
Arteta anaamini ifikapo mwisho wa msimu watakuwa na uhuru wa kuchagua mchezaji wanayemuhitaji na wanaamini kwamba huenda wakalipa kiasi kidogo cha pesa tofauti na ilivyo sasa ambapo timu nyingi zinahofia kuuza mastaa wao kwa sababu ligi bado zinaendelea na hata zile zilizo tayari kuwauza zimekuwa zikihitaji kiasi kikubwa cha pesa.