Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametembelea Dahalia la Wavulana Skuli ya Sekondari Kengeja, ambayo iliungua moto usiku Januari 31, 2024, Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Akiwa mahala hapo, Dkt. Mwinyi amewafariji Wanafunzi na Walimu wa Skuli hiyo ya Kengeja na kuahidi kuijenga upya pamoja na dahalia iliyoungua moto.
Awali, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa aliwashukuru wadau mbalimbali waliojitolea michango akiwemo msamaria mwema aliyejitolea shilingi milioni 300 na Mfanyabiashara Rostam Aziz aliyetoa milioni 100.
Rais Dkt. Mwinyi aliwasili uwanja wa ndege wa Pemba na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Mattar Zahor Masoud na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Dini, Chama cha Mapinduzi na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, ambapo pia ameyashukuru makampuni, wadau mbalimbali waliojitokeza na kuchangia misaada mbalimbali kwa ajili ya shule hiyo.