Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kenya ‘FKF’, Sam Nyamweya amesifu kiwango cha timu ya taifa ya Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’.

Taifa Stars ilikuwa timu pekee kwenye ukanda wa Afrika Mashariki kwenye michuano hiyo iliyojumuisha mataifa 24.

Ikiongozwa na Nahodha wake Mbwana Samatta na nyota wengine kama vile Feisal Salum, Mlinda Lango Aisha Manula na Simon Msuva, Stars ilipata sare mbili kwenye mashindano hayo.

Pamoja na matokeo hayo, Nyamweya anaamini Tanzania ilionesha kiwango bora kwenye mashindano hayo yanayoendelea nchini Ivory Coast.

“Ingawa hawakuvuka hatua ya makundi, kiwango chao kilikuwa bora, walionyesha kukomaa na ni dalili nzuri kwa baadae,” amesema Nyamweya.

“Japo walipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Morocco, Tanzania walikaribia kupata ushindi kwenye mechi yao dhidi ya Zambia na walitoka sare mechi yao ya mwisho na DR Congo.

“Nawaomba Jumuiya ya Afrika Mashariki kuweka mkazo kwenye AFCON ya mwaka 2025 na ile ya mwaka 2027, ambayo itaandaliwa na Tanzania, Kenya na Uganda kwa pamoja. Mkazo tuweke kwenye maandalizi na hii iendane na kuimarisha vikosi vyetu.”

WFP, Serikali kutumia teknolojia ushughulikiaji maafa
Kamati ya Bunge yaridhishwa ubora wa huduma BMH