Mshambuliaji wa Kikosi cha Timu ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ Nigeria Victor Osimhen, hakuwa katika msafara wa ulioelekea mjini Bouake nchini Ivory Coast, kwa ajili ya mchezo wa Nusu Fainali ya AFCON 2023.

Nigeria itakipiga dhidi ya Afrika Kusini kesho Jumatano (Februari 07) ili kumsaka mshindi atakayetinga mchezo wa Fainali utakaopigwa mwishoni mwa juma hili.

Taarifa kutoka ndani ya Timu ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ zimeeleza kuwa kabla ya kikosi kuanza safari ya kuelekea Bouake, Mshambuliaji huyo wa SSC Napoli ya Italia alikuwa hajisikii vizuri kutokana na tatizo la tumbo na angesalia mjini Abidjan akisubiri kibali cha matibabu.

Kulingana na taarifa hiyo: “Victor Osimhen hatajiunga nasi katika safari hii kutokana na maumivu ya tumbo. Madaktari wa timu walithibitisha kuwa amewekwa chini ya uangalizi wa karibu na mshiriki wa timu ya matibabu iliyobaki huko Abidjan pamoja naye.

“Iwapo ataruhusiwa kufikia kesho asubuhi (Jumanne), ataungana na wachezaji wengine kabla ya saa kumi na moja jioni.”

Haijulikani ni nini kimemsababishia maumivu ya tumbo Osimhen, ingawa Mshambuloiaji huyo alionekana kupigwa na butwaa alipotolewa katika mchezo wa Robo Fainali dhidi ya Angola.

Kumpoteza Mchezaji Bora wa Kiafrika wa sasa itakuwa pigo kubwa kwa Nigeria, ambayo mashambulizi yake yamesimama kwenye harakati za hali ya juu za mshambuliaji huyo.

Osimhen amehusika katika mabao manne kati ya sita ya Nigeria hadi sasa kwenye michuano hiyo, ikiwa ni pamoja na kufunga bao pekee katika sare ya kwanza ya 1-1 dhidi ya Equatorial Guinea.

Iwapo hatoweza kufika kwa wakati kwa mchezo huo, kocha Jose Peseiro ana chaguo katika Kelechi Iheanacho wa Leicester City, Paul Onuachu wa Trabzonspor, na Terem Moffi wa OGC Nice.

Onuachu amekuwa mbadala wa Osimhen katika michuano hiyo, huku Iheanacho na Moffi wakiwa bado hawajapata dakika zozote.

Wabunge waridhia kuahirisha uchaguzi, Upinzani wapinga
Kamati FECAFOOT yamkatalia Eto'o