Kiungo kutoka nchini Zambia na Klabu ya Simba SC, Clatous Chama amesema amesahau yaliyopita na yupo nchini kwa ajili ya kuitumikia na kuipa mataji timu hiyo bila kinyongo.

Akizungumza na moja ya televisheni za mtandaoni, Chama amesema anatambua maneno mengi yamesemwa lakini anaushukuru uongozi wa Simba SC kwa kukubali msamaha wake.

“Nipo hapa kwa ajili ya kuipigania Simba SC kubeba mataji katika mashindano yote, changamoto za hapa na pale ni vitu vya kawaida kwenye kazi, nafurahi yamepita na sasa nipo kazini,” amesema Chama.

Kiungo huyo amesema hataki kuendeleza malumbano ambayo hayana msingi sababu suala la msingi limemalizika na yeye yupo kazini.

Amesema atashirikiana na wachezaji wenzake ili kuisaidia timu hiyo kurudisha taji la ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la ASFC na kufika Nusu Fainali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Amesema kwa ushindani uliokuwepo anajua haitakuwa rahisi lakini kwa ubora wa benchi lao la ufundi na uwezo waliokuwa nao wachezaji anaamini hakuna kitakachoshindikana.

Chama alisimamishwa na uongozi wa timu hiyo yeye na Nassoro Kapama kwa madai ya utovu wa nidhamu lakini baadae yeye alirudishwa kundini baada ya kuomba msamaha kwa viongozi na Benchi la Ufundi la timu yake.

Uwekezaji: Makala aikaribisha NSSF Uwanja wa Ndege Mwanza
Dabo ahimiza mabao zaidi Azam FC