Kiungo Mshambuliaji ‘WINGA’ kutoka Afrika Kusini na Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’, amesema amegundua mbinu mpya ya kupata muda zaidi wa kucheza kikosini.
Skudu aliyeanza kukitumikia kikosi hicho msimu huu akitokea Marumo Gallants ya kwao, pia amezungumzia timu yao ya Taifa ‘Bafana Bafana’ inavyofanya vizuri kwenye Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’.
Kuhusu Young Africans, amesema kuwa nafasi yake bado anaendelea kuipambania ndani ya kikosi hicho licha ya ushindani mkubwa wa namba uliopo lakini anaamini kwasasa njia zimefunguka na ameshajua cha kufanya kuongeza wigo wake.
Amekiri kuwa kutokana na ubora wa wachezaji waliopo katika timu hiyo, sio jambo jepesi kupata muda mwingi wa kucheza, lakini amerudi raundi ya pili ya msimu na mbinu mpya kabisa ili kuhakikisha anatoboa na haoni kitakachomzuia.
“Kwa ushindani uliopo nimegundua kuwa ili niweze kuwa na nafasi zaidi lazima nifanye kitu cha tofauti kila ninapopata nafasi.
Kila Kocha atakaponipa nafasi lazima nionyeshe kuwa nilistahili kwa kufanya jambo ili mwalimu anipe namba zaidi,” ameongeza kuwa tayari pia ameshaizoea ligi tofauti na awali.
Aidha, ameeleza kama utani timu yao ya Bafana Bafana imepasua na watu wasishangae wakichukua taji la Afrika kwani wana kipa na kikosi bora sana.
“Kipa tuliyenaye namfahamu. Timu ya Taifa na kikosi cha Mamelodi kimekuwa kwenye mapambano ya kumsuka kufikia kiwango hicho alichonacho, ni mzuri sawa na Diigui Diarra” amesema.