Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi amesema katika makipa watano Bora kwenye Fainali za Mataifa ya Bara la Afrika ‘AFCON 2023’ zinazoendelea nchini Ivory Coast, Djigui Diarra yumo.

Diarra alicheza mechi zote za ‘AFCON 2023’ katika timu yake ya Taifa ya Mali, mpaka walipotolewa hatua ya Robo Fainali dhidi ya Ivory Coast dakika za mwishoni.

Anaporejea katika kikosi chake cha Young Africans keshokutwa Alhamisi (Februari 08), kocha wake Gamondi amempongeza pia Aziz KI kwa kiwango kizuri ingawa hajafunga bao lolote ila hakuwasahau wachezaji wa Taifa Stars amesema walifanya kazi nzuri.

“Ndani ya kikosi changu Diarra ni shujaa kwa hatua ambayo amefika na Taifa lake la Mali ninaamini mashabiki wa timu hiyo watampokea kwa heshima.

“Wachezaji sasa wanarejea klabuni kwao wanatakiwa kusahau kuhusu matokeo ya ‘AFCON 2023’ na badala yake waendeleze makali yao na kama wamelikosa taji la ‘AFCON 2023’ basi watapata wakiwa na Young Africans,” amesema Gamondi.

Diarra katika michuano hiyo amecheza dakika 450. Katika mechi hizo ameruhusu jumla ya mabao manne huku timu yao ikiwa imefunga jumla ya mabao 6 katika michezo mitano.

Taarifa zinzeleza kuwa Simu zimeanza kuita kwa kipa huyo kutokana na uwezo mzuri aliouonyesha, hivyo huenda baada ya msimu huu Young Africans watakuwa na kibarua kigumu kuweza kushindana na vigogo kumbakiza mchezaji huyo.

Diarra, kipa namba moja wa Young Africans, alifanya kazi kubwa msimu uliopita na kuifikisha timu hiyo kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Ajali ya Moto: Wafanyabiashara Mbuyuni wapewa neno la faraja
Skudu: Nimejitafuta, nimejipata