Kocha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Hugo Broos ameliweka soka la Afrika Kusini katika ramani ya dunia, lakini ameonya kwamba Ligi Kuu ya nchi hiyo inapaswa kuboreshwa ili kuinua vipaji vya nyumbani.
Kauli hiyo ya Broos ni kama jibu kwa waliokuwa wakimponda kwa kuipeleka Bafana Bafana katika Nusu Fainali yao ya kwanza katika miaka 24.
“Kwa hiki kilichotokea soka la Afrika litaanza kuchukuliwa siriaz, lakini Ligi Kuu ya PSL bado inatakiwa kuboreshwa,” amesema.
Kocha huyo mzaliwa wa Ubelgiji amesema kiwango kilichoonyeshwa na Bafana Bafana hadi kufika Nusu Fainali yao ya kwanza tangu 2000, ni picha halisi ya Ligi Kuu ya PSL kwa sababu wachezaji 20 kati ya 23 alioenda nao kwenye ‘AFCON 2023’ wanacheza soka la ndani nchini Afrika Kusini. Hata hivyo, Broos amesema PSL bado inapaswa kuwa bora zaidi.
Broos amekuwa akiwaanzisha hadi wachezaji wanane wa klabu ya Mamelodi Sundowns katika kikosi cha kwanza cha timu ya taifa ya Afrika Kusini huku pia akimjumuisha mchezaji wa tisa, Percy Tàu, ambaye pia ameitumikia Mamelodi kabla ya kutua kwa mabingwa wa Afrika, AI Ahly ya Misri.
“Tumekuja hapa na nadhani kulikuwa na watu wengi sana kule Afrika Kusini ambao hawakuwa na imani na timu hii, lakini sisi tuliiamini. Wachezaji waliamini kwamba inaweza kuwa na imekuwa,” Broos amekaririwa na televisheni ya SABC Sport.
“Nadhani hili ni jambo zuri sana kwa soka la Afrika Kusini. Wachezaji wa Afrika Kusini wako sokoni sasa, hivyo inamaanisha kwamba soka la Afrika Kusini litaangaliwa zaidi,” ameongeza.
Bafana Bafana itaivaa Nigeria katika Nusu Fainali kesho Jumatano (Februari 07).