Kocha wa DR Congo, Sebastien Desabre anaamini kikosi chake kina nafasi nzuri zaidi ya kutwaa ubingwa wa Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ baada ya kufika Nusu Fainali.

DR Congo inayoundwa na wakali kibao akiwamo beki wa Simba SC, Henick Inonga, iliifunga Guinea 3-1 Ijumaa (Februari 02) na kutinga Nusu Fainali ambako sasa itakutana na wenyeji Ivory Coast.

Timu hizo mbili zitakutana kwenye Uwanja wa Olympique Alassane Ouattara, huku DRC mara ya mwisho kutwaa taji la AFCON ilikuwa mwaka 1974.

Wenyeji Ivory Coast walitwaa taji hilo mara ya mwisho mwaka 2015 na wamedhamiria kulibeba tena mbele ya mashabiki wao.

“Itakuwa ni ujinga kuacha kuamini kwamba tutashinda fainali. Lakini itakuwa ni ngumu. Tuna washambuliaji kama (Cedric) Bakambu, (Simon) Banza na Mayele Fiston. Tunajua kwamba ni ishu ya muda tu kabla hatujatwaa ubingwa.

“Unapofika Nusu Fainali, jambo la kwanza unataka kufika Fainali. Na kama ukiweza kufika fainali, unataka kushinda ubingwa. Tutafanya kila kitu kutwaa ubingwa huu, hatuna cha kujutia.”

Kabla ya kukabiliana na Guinea, Chui wa Congo walitoka sare tatu katika hatua ya makundi 1-1 dhidi ya Zambia, 1-1 dhidi ya Morocco na 0-0 dhidi ya Taifa Stars ya Tanzania.

Kwenye hatua ya l6-Bora, pia DR Congo ilitoka sare ya 1-1 dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo, Misri kabla ya kuwaondoa Mafarao hao kwa Penati 8-7.

Wacongo walianza kuwa watamu katika hatua ya Robo Fainali ambako waliichakaza Guinea 3-1.

“Ubora huu umekuja muda mwafaka wakati tunalikaribia kombe.” amesema kocha Desabre.

Simba, Young Africans zarudishwa Kwa Mkapa
12,500 Tunduru kunufaika Mradi wa Maji Mbesa - Lijombo