Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro, amesena kuwa licha ya kuufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa kupisha ukarabati, utaendelea kutumika kwa baadhi ya michezo mikubwa hasa inayohusisha Young Africans, Simba SC na timu za Taifa.
Akizungumza na jijini Dar es Salaam Ndumbaro amesema baadhi ya mitandao ya kijamii imekuwa ikipotosha suala hilo kuwa uwanja huo umefungwa kupisha ukarabati na kwamba usingetumika kwa mechi zote mpaka utakapokamilika.
“Ukweli ni kwamba ukarabati bado unaendelea Uwanja wa Benjamini Mkapa lakini hiyo haina maana kuwa hakutafanyika mechi yoyote, kuna baadhi ya mechi kubwa zinazozihusisha Young Africans, Simba SC na Taifa Stars zitachezwa kwenye uwanja huu. Haya ndio maamuzi yetu ya tangu zamani sio ya leo.
“Mchezo kama wa Young Africans na Simba SC hauwezi kuupeleka kwenye uwanja mdogo, utaua watu na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan haikusudii hilo kutokea,” amesema Ndumbaro.
“Tuliishasema tangu awali michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika na michezo ya timu za taifa zitacheza Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa sababu dimba hilo ndilo pekee lililoidhinishwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) hapa nchini.
Amesema hawana maombi kutoka timu yoyote lakini hayo ni maamuzi ya wizara yake baada ya kukaa na wadau wengine na kwa sababu huo ndio uwanja ulioidhinishwa na CAF, usipotumika huo hakuna mwingine maana ili upatikane mwingine lazima uite maafisa wa CAF waje kukagua na waridhie.