Wakurugenzi wa Wizara za Sekta mbalimbali na Taasisi za Umma, wametakiwa kuwa na mkakati wa kuwezesha utekelezaji wa mipango na bajeti za kisekta, ili iwe na tija katika kuboresha utoaji wa huduma kwa Wananchi.
Wito huo, umetolewa jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Sospeter Mtwale wakati akifungua kikaokazi cha kujadili mipango na bajeti za wizara za kisekta kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kilichowahusisha wakurugenzi wa wizara, taasisi pamoja wataalam.
Amesema, washiriki wa kikao kazi hicho wanatakiwa kujadiliana kuhusu maandalizi ya mipango na bajeti za wizara za kisekta za mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuweka mazingira bora ya utekelezaji wake kwa kuzingatia maslahi mapana ya taifa na ustawi wa jamii.
“Mipango na bajeti za utekelezaji wa kisekta inapaswa kuwekewa mkakati mahususi wa pamoja ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wake katika ngazi za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa,” alisema Mtwale.
Aidha, aliongeza kuwa, utelezaji wa miradi na shughuli za kisekta katika mamlaka za serikali za mitaa baadhi ya maeneo umekuwa na changamoto kwasababu ya kutokuwa na uratibu mzuri katika maandalizi na utekelezaji wake hivyo amewata washiriki kuweka utaratibu wa kutatua changamoto hiyo.