Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ imefikia Nusu Fainali ambako Nigeria itaivaa Afrika Kusini saa 2:00 usiku na wenyeji Ivory Coast dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) saa 5:00 usiku leo Jumatano (Februari 07).

Bafana Bafana wanakutana na mahasimu wao wa zamani, Nigeria katika Nusu Fainali ya kwanza katika kile kitakachokuwa ni marudio ya Nusu Fainali ya mwaka 2000 ambayo ilishuhudia Super Eagles wakiwafunga mabingwa hao wa 1996 kwa mabao 2-0 mjini Lagos.

Ushindani kati ya pande hizo mbili ni muhimu kwani Nigeria itakuwa ikisaka taji lao la nne, wakati Afrika Kusini ikitazamia kutwaa taji la pili.

Baada ya kushindwa kwa Nusu Fainali ya 2000, Super Eagles waliwabwaga Bafana Bafana kwenye hatua ya Robo Fainali mwaka  2019 nchini Misri kwa mabao 2-1.

Timu zote mbili zimekutana mara 14, huku Super Eagles wakiongoza kwa ushindi mara saba dhidi ya mara mbili wa Afrika Kusini, huku mechi tano zikitoka sare.

Hii itakuwa mechi nyingine muhimu katika historia ya soka ya Afrika, huku Bafana Bafana wakiwa chini ya makocha wawili wa zamani waliowahi kushinda ubingwa wa Afrika wakikabiliana na kikosi cha Super Eagles kilichoshiba nyota.

Afrika Kusini inaongozwa na kocha mshindi wa AFCON 2017, Hugo Broos aliyewaongoza Cameroon kushinda ubingwa miaka mitano iliyopita.

Broos raia wa Ubelgijl anasaidiwa na Helman Mkhalele mchezaji muhimu wa kizazi cha dhahabu cha 1996 kilichobeba taji la kwanza na pekee la Afrika Kusini.

Itakuwa mechi ngumu dhidi ya Super Eagles wanaoongozwa na mshambuliaji hatari, Victor Osimhen na Ademola Lookman mwenye kasi.

Uwanja Azteca kufungua Kombe la Dunia 2026
Makala: Kesho ni fumbo wakati sahihi ni leo