Gwiji wa soka nchini Ghana, Michael Osei amefunguka kuhusu mtazamo wake kwa nini anaona Mlinda Lango Richard Ofori hakupaswa kujumuishwa kwenye kikosi cha ‘AFCON 2023’.
Ghana, mabingwa mara nne wa ‘AFCON 2023’, waliondolewa kwa aibu katika Hatua ya ya makundi mwaka huu, baada ya sare isiyotarajiwa ya 2-2 dhidi ya Msumbiji katika mechi yao ya mwisho ya Kundi B.
Chama la Ofori lilimaliza nafasi ya tatu Kundi B, likishindwa kupata ushindi hata mmoja. Waliishia kupata sare mbili dhidi ya Misri na Msumbiji lakini wakakutana na kichapo mikononi mwa Cape Verde.
Kocha wa Ghana, Chris Hughton alichagua kumtumia kipa Ofori anayedakia Orlando Pirates na kuwaacha nje Lawrence Ati-Zigi na Joe Wollacott, ambao wote wanacheza soka Ulaya.
“Ukweli ni kwamba Richard Ofori ni kipa mzuri sana, pia anacheza katika moja ya klabu kubwa Afrika, lakini hakuwa tayari kwa ajili ya AFCON 2023,” aliiambia tovuti ya FARPost.
“Lawama zinapaswa kwenda kwa kocha na benchi lake la ufindi. Wao ndio wanaopaswa kulaumiwa kwa kumchezesha. Tungeweza kufanya vyema zaidi ya tulivyofanya. Ofori hakuwa fiti kwa ajili ya michuano hii. Ndio, namuamini, lakini hakuwa fiti. Alifanya makosa ya kizembe sana kwa sabau alikuwa hajacheza mechi kwa muda mrefu.
“Wakati mwingine unahitaji kujenga kujiamini kwa kucheza mechi nyingi kabla ya kwenda kwenye michuano mikubwa. Hakuwa tayari na namlaumu kocha kwa kumchezesha katika michuano muhimu kama hii,” ameongeza.
Akienda kwenye AFCON 2023, Ofori alicheza mechi tatu tu za Orlando Pirates katika michuano yote ya msimu huu wa 2023/24.
Katika mechi tatu za AFCON 2023, Mlinda Lango huyo mwenye umri wa miaka 30, aliruhusu mabao sita, akionyesha kiwango cha kufadhaisha langoni.