Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema dunia inaenda kwenye maendeleo makubwa ya matumizi ya mifumo ya kielektroniki na umma umeanza kuelimishwa juu ya matumizi hayo, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya mifumo hiyo kwa kukashifu na kudhalilisha watu wakiwemo watoto na wanawake.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje, aliyetaka kufahamu Serikali imejipangaje kuhakikisha inatengeneza mazingira bora ya kisera na kisheria ya ulinzi wa watoto mtandaoni. Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kuhamasisha matumizi sahihi ya mitandao hiyo.
Amesema, “hata tulivyokuwa tunapitisha Muswada wa Vyama vya Siasa tumelizungumza hili na tumeliwekea kibano kwa wale watakaotumia vibaya mitandao kwa ajili ya kudhalilisha watu kwenye eneo la siasa. Pia Serikali imeweka mkakati wa kukabiliana na unyanyasaji, vitendo vya ukatili kwa watoto, wanawake na makundi mengine.”
Aidha, Waziri Mkuu pia amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jansia, Wanawake na Makundi Maalumu imeweka utaratibu wa kukabiliana na wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kudhalilisha watu na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha udhibiti wa matumizi mabaya ya mitandao kwa kuwachukulia hatua kali wote watakaobainika kufanya hivyo.