Wilaya ya Mbeya, inatarajia kuanza uchomaji wa Chanjo ya sindano ya kupambana na ugonjwa wa Surua na Rubella, kwa watoto 133,438 walio katika umri wa miezi 9 mpaka chini ya miaka 5 katika Halmashauri zake mbili.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua kampeni hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewaomba Viongozi wa Dini ,Watu mashuhuli na Viongozi wa Kimila kuendeleza ushirikiano waliouonesha wakati wa kampeni na zoezi la chanjo ya Polio mpaka kufikia kuvuka malengo.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amewaomba Viongozi wa Dini ,Watu mashuhuli na Viongozi wa Kimila kuendeleza ushirikiano waliouonesha wakati wa kampeni na zoezi la chanjo ya Polio.

Amesema, pia Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wanatakiwa kuhakikisha wanafikisha ujumbe na elimu juu ya chanjo hiyo, ili kuepusha kujitokeza kwa uzushi na imani potovu wakati wa kampeni na zoezi la Chanjo hiyo ambayo hutolewa dozi mbili pale mtoto anapofikisha umri wa miezi 9 na miezi 18.

Wakati wa zoezi la Chanjo ya Surua na Rubella, Watoto 68,660 watachanjwa katika Halmashauri ya Jiji la Mbeya na Watoto 64,788 watachanjwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, huku kampeni hiyo ikitarajiwa kufanyika nchi nzima kuanzia Februari 15-18, 2024 katika vituo vya kutolea huduma za chanjo na maeneo maalum yaliyoandaliwa.

Lengo kuu la kampeni hiyo ni kuzuia kuenea kwa ugonjwa Surua na Rubella na kuongeza kinga kwa walengwa hata kama wameshapata chanjo katika utaratibu wa kawaida wa kutoa huduma za chanjo.

Surua ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa kwa njia ya hewa, dalili zake ni pamoja na Homa, mafua, Kikohozi, macho kuwa mekundu na kutoa majimaji na vipele vidogo vidogo ambavyo huanza kujitokeza kwenye paji la uso, nyuma ya masikio na kusambaa usoni na mwili mzima na hukingwa kwa chanjo ya Surua.

Super Eagles yamfurahisha Saka
Kamanda Pasua aiongoza STPU upandaji Miti Monduli