Shirikisho la Soka nchini Mauritania, limefikia makubaliano na Kocha Amir Abdou kusaini mkataba mpya utakaomfanya aendelee kuinoa timu ya taifa ya nchi hiyo hadi mwaka 2026.
Uamuzi huo umefanyika baada ya Mauritania kuridhishwa na kazi nzuri iliyofanywa na Abdou kwa kuiongoza timu yao ya taifa kutinga hatua ya 16 bora ya fainali za mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ mwaka huu na walitolewa na Cape Verde kwa kufungwa bao 1-0.
Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza kwa timu ya taifa ya Mauritania kutinga katika hatua hiyo baada ya kuishia hatua ya makundi ya mashindano hayo mwaka 2019 na 2021.
Mkataba wa awali wa Abdou na Mauritania ulikuwa umalizike mwaka huu lakini sasa kocha huyo atadumu na timu ya taifa ya nchi hiyo kwa miaka mwili zaidi.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Mauritania linatangaza limefikia makubaliano na kocha wa timu ya taifa, Amir Abdou kuongeza mkataba wake kama kocha wa timu ya taifa hadi 2026,” imeeleza taarifa ya shirikisho hilo.
Mbali na kutinga hatua ya 16, Amir Abdou pia aliiongoza Mauritania kupata ushindi wake wa kwanza kwenye ‘AFCON 2023’ baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Algeria ambao ulikuwa ni wa Kundi D.
Jukumu la Abdou kwa sasa ni kuiongoza Mauritania katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia 2026, pia kuwania kufuzu fainali zijazo za Barani Afrika ‘AFCON 2025’.