Klabu ya Santos ya Brazil ina mpango wa kumrudisha Kiungo Mshambuliaji ‘WINGA’ Neymar, baada ya kupona majeraha na kujiunga katika timu ya Al Hilal ya Ligi Kuu ya Saudi Arabia.
Neymar alisajiliwa Al Hilal katika usajili wa majira ya kiangazi, mwaka jana kwa uhamisho wa paini milioni 78, hivi sasa yupo nje ya dimba akiuguza jeraha la goti.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32, aliyeumia wakati akiwa na timu ya taifa ya Brazil, anatarajiwa kukosa msimu mzima baada ya kufanyiwa upasuaji wa kutibu jeraha lake.
Mkataba wa sasa wa mchezaji huyo katika kikosi cha Al Hilal unatarajiwa kumalizika mwakani, lakini tayari klabu ya Santos imeshapanga kuinasa saini ya mshambuliaji wake huyo wa zamani.
Rais wa Santos, Marcelo Teixeira, tayari ameanza mazungumzo na wakala wa Neymar na imeelezwa wapo katika hatua nzuri.
“Mazungumzo ya kumsajili Neymar yalikuwa ya haraka, lakini mara zote mazungumzo ya haraka yana matokeo mazuri. Kurudi na kucheza hapa, anahitaji kuwa fiti na majeraha. Ataendelea kuwa Saudi Arabia na baadae atarejea hapa,” amesema.
Awali, Neymar alikipiga Santos kuanzia mwaka 2009 hadi 2013 alipotimkia FC Barcelona kabla ya baadae kutua Paris Saint-Germain ya nchini Ufaransa.