Kocha Mkuu wa Coastal Union, David Ouma ameonyesha matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC FC utakaopigwa baadae leo Jumatatu (Februari 12) kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es salaam.

Ikumbukwe kabla ya Ligi kusimama kupisha mashindano ya AFCON 2023, Coastal mechi yake ya mwisho ilikuwa ni dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania katika uwanja huo huo wa Azam Complex Desemba 18 mwaka jana ambapo kikosi hicho kilishinda bao 1-0.

KMC yenyewe inarudi tena katika uwanja huo huo kuendeleza pale ilipoishia ambapo mara ya mwisho ilitoka sare ya mabao 2-2, dhidi ya Simba SC Desemba 23, mwaka jana.

Ouma amesema anatambua wanaenda kukutana na timu ngumu iliyofanya maandalizi ya kutosha na mabadiliko kadhaa dirisha dogo hivyo amejipanga kutoa ushindani na kuondoka na pointi tatu.

“Tuko vizuri na kila kitu kiko sawa kwa sababu vijana wako katika ari na morali nzuri ya kupambana na kushinda ambapo hayo ndio malengo yetu,” amesema Ouma.

Kocha huyo ameongeza malengo yao ya kumaliza nafasi za juu bado yapo palepale ndio maana dirisha dogo la usajili alifanya mabadiliko kwa kuwaleta washambualiaji wenye uwezo mkubwa akiwemo Salim Aiyee (Mbuni FC) na Crispin Ngushi kutoka Young Africans.

KMC inashika nafasi ya nne na Pointi 21 tofauti ya mbili na Coastal Union iliyopo ya sita na Pointi 19, zote zikicheza michezo 14.

Hugo Broos awapongeza wachezaji wake
Wananchi jengeni utaratibu wa kupima afya - Mchengerwa