Mshambuliaji kutoka nchini England, Harry Kane atamkaribisha kwa mikono miwili Kocha Jose Mourinho huko Bayern Munich, baada ya wawili hao kuwa na uhusiano mzuri walipokuwa pamoja Tottenham Hotspur.

Mourinho anahusishwa na mpango wa kwenda kujiunga na miamba hiyo ya Ujerumani baada ya sasa kutokuwa na kazi tangu afutwve kazi huko AS Roma, huku Kocha wa Bayern Munich, Thomas Tuchel akiwa kwenye presha kubwa kutokana na timu kushindwa kufanya vizuri.

Bayern kwa sasa ipo nyuma kwa pointi tano kwenye msimamo wa Bundesliga na vijana Bayer Leverkusen baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa kikosi hicho cha Xabi Alonso, mwishoni mwa juma lililopita (Jumamosi – Februari 10).

Matarajio ni makubwa huko Bayern hasa baada ya sasa Mourinho akiwa anapatikana sokoni, kitu ambacho kinawafanya mabosi wa miamba hiyo ya Allianz Arena kukuna vichwa wakitafuta namna ya kupata huduma yake.

Na kinachoelezwa, Mourinho ameshaanza kujifunza Kijerumani, akisubiri Tuchel afukuzwe.

Kane alionekana kuchukizwa na kiwango cha Bayern kwenye mechi yao dhidi ya Leverkusen na aliwalaumu wachezaji wenzake kwa kupoteza mipira na kujiweka kwenye presha kubwa.

Nahodha huyo wa England amejiunga na Bayern akiwa na matumaini ya kunyakua mataji baada ya kushindwa kufanya hivyo alivyokuwa Spurs.

Mourinho alimnoa Kane huko Spurs kuanzia Novemba 2019 hadi 2021 na walikuwa na uhusiano mzuri na katika kipindi hicho, Mshambuliaji huyo alifunga mabao 45 na asisti 18 katika mechi 62.

Kane alisema: “Nadhani na Jose tumekuwa na uhusiano mzuri, tulielewana kuanzia dakika ya kwanza tu.”

Kamati ya Bunge yapongeza Teknolojia mpya ya ufundishaji
Serikali yakanusha Madiwani kukopwa Posho