Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Hamduni, amewaambia Wanachama na Mashabiki wa Simba SC kuwa wamesikia kilio chao dhidi ya mwamuzi Ramadhani Kayoko na jambo hilo litakwenda kufanyiwa kazi na Kamati ya Nidhamu, huku uwezekano wa kuadhibiwa ukiwa mkubwa endapo itathibitika alikuwa na mapungufu kwenye uamuzi wake.

Siku ya ljumaa (Februari 09) baada ya mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Azam FC kumalizika, mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi hao walifanya maandamano ndani ya uwanja wa CCM Kirumba, wakimshutumu mwamuzi huyo kwa kutochezesha mechi hiyo kwa haki, wakidai aliwanyima haki kwenye baadhi ya matukio na kuwafanya kutoka sare ya bao 1-1.

Akizungumza jijini Dar es salaan, Hamduni amewaomba radhi mashabiki na wadau wote waliokwazwa kwa njia moja ama nyingine kutokana na ufanyaji kazi wa waamuzi katika mechi za hivi karibuni ambazo zimeonekana kuwa na malalamiko mengi.

“Tumeyasikia, tunaheshimu kauli za mashabiki kwa sababu hao ndio wadau wetu wa soka na ‘waswahili’ wanasema ndiyo wanaotuweka mjini, tumesikia na naomba kuwaeleza.

“Suala la kukataa mwamuzi si la mashabiki, viongozi au kamati yetu waamuzi, bali lipo kwenye kamati maalum ambayo inachunguza mwenendo wa waamuzi, na kama Kayoko ataonekana ana matatizo kwenye mechi aliyochezesha atachukuliwa hatua nasi yeye tu, yeyote yule ambaye itabainika amevurunda, tunaomba mashabiki watulie wasubiri Kamati ya Nidhamu ambayo imeshajua hayo, watachukua hatua, na sisi Kamati ya Waamuzi ikitufikia tutaridhika kwa maamuzi watakayochukua,” amesema.

Mwenyekiti huyo amewaomba radhi mashabiki na wadau wote wa soka ambao wamekwazwa na tukio hilo au linguine ambalo limesababishwa na kile ambacho wanaona waamuzi hawakutenda sawa.

“Napenda kuwapa pole wadau wote wa soka ambao wamekwazwa kwa njia moja ama nyingine kutokana na ufanyaji kazi wa waamuzi, sisi kama Kamati ya waamuzi kwanza lengo letu kuwapanga waamuzi tu, si kwenda kuharibu mchezo, wala kuwanyima watu mabao au kuwapendelea watu, kwa hiyo sisi tutaendelea kushirikiana na Shirikisho la Soka nchini ‘TFF’, kuhakikisha waamuzi wetu wanakuwa bora zaidi na hii ni kuwapa elimu na kueleza makosa yao yote,” amesema.

Lionel Messi kucheza olimpiki 2024
Kamati ya Bunge yapongeza Teknolojia mpya ya ufundishaji