Michezo ya timu ya Simba SC ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara, inatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Simba SC imetangaza kutumia uwanja Jamhuri kuwa dimba lake la nyumbani baada ya viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru, ilivyokuwa ikivitumia kufungwa kwa lengo la kufanyiwa ukarabati.
Timu hiyo itautumia uwanja Jamhuri baada ya kufunguliwa kufuatia kumalizika kwa marekebisho mbalimbali ikiwema sehemu ya kuchezea, vyumba ya kubadilishia nguo na mapumziko kwa wachezaji.
Kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi kitakuwa mjini Morogoro baada ya kucheza mechi za ugenini jijini Mwanza, Kigoma na Tabora.
Simba SC ilianza kusaka alama tatu mkoani Kigoma dhidi ya Mashujaa na kushinda bao 1-0 kabla ya kuichapa Tabora United mabao 4-0 katika uwanja wa Ali Hassan, Tabora.
Kisha iliikaribisha Azam FC katika uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kutoka sare ya ba 1-1 kabla ya juzi Jumatatu (Februari 12) kushinda bao 1-0 dhidi ya Geita Gold, katika uwanja huo huo.
Mratibu wa Simba SC, Abbas Ally, amesema taratibu za kuutumia Uwanja wa Jamhuri zipo katika hatua za mwisho, na tayari uongozi umewasilisha barua Bodi ya Ligi ‘TPLB’ kwa lengo la kuijulisha kuhama katika dimba hilo.
Wakati Simba SC ikiichagua Uwanja huo, Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Mwakasungula, amesema mchezo wao dhidi ya Young Africans utachezwa katika dimba hilo.
KMC FC itakuwa mwenyeji katika mchezo huo wa 16 utakaofanyika Jumamosi (Februari 17).