Chama cha Soka nchini Rwanda ‘FERWAFA’ kimemsimamisha kwa muda kucheza soka nchini humo mchezaji wa kimataifa wa Congo Héritier Luvumbu kwa kuonyesha ishara ya kisiasa wakati wa mchezo wa Ligi Kuu mwishoni mwa juma lililopita.
Mchezaji huyo raia wa Congo anayechezea klabu ya Rayon Sport ya Rwanda anadaiwa kuonyesha ishara hiyo wakati timu yake ilipokuwa ikicheza dhidi ya timu ya Polisi ya Rwanda ‘Polisi FC’, Jumapili (Februari 11).
Inasemekana Héritier Luvumbu alionekana akifunga mdomo wake kwa mkono wake wa kushoto, huku akielekeza vidole vyake viwili kichwani, baada ya kufunga bao.
Ishara hiyo hiyo inalenga kukemea ukimya wa Jamii ya Kimataifa kuhusu mauaji ambayo yamekuwa yakifanyika nchini mwake, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Serikali ya DRC inailaumu Rwanda kama nchi inayotoa msaada kwa moja ya makundi makuu ya waasi yaliyoteka maeneo ya Mashariki mwa DRC, M23
Tuhuma kama hizo pia zimeungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lakini Rwanda inakanusha kuhusika na mzozo huo.
Ishara hiyo pia kilionyeshwa na Timu ya Taifa ya DRC katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, wakati ikicheza dhidi ya wenyeji, Ivory Coast wakati wa Nusu Fainali, tarehe 7 Februari 2024.
Héritier Luvumbu anadai kuwa ishara hiyo imemfanya akemewe mtandaoni, na sasa ana wasiwasi kuhusu usalama wake nchini Rwanda.
Kabla ya kuondoka DRC, mshambuliaji huyo alikuwa akiichezea AS Vita Club, iliyoanzishwa mwaka 1935 na klabu moja kongwe ya soka katika mji mkuu Kinshasa.
Taarifa za hivi punde zinasema kuwa Rayon Sports inasema imeachana na kiungo wa zamani wa Congo, Nzinga Luvumbu.
Rayon Sports inasema kuwa uamuzi huo ulifanywa “Kwa makubaliano ya pande zote mbili”, lakini ulitokea baada ya shirikisho la soka nchini Rwanda ‘FERWAFA’, kumuadhibu Luvumbu kwa kusimamishwa kwa miezi sita kwa ‘ishara za kisiasa’ uwanjani.