Licha ya kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu kwa ushindi wa mabao 3-2 ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar, Kocha Mkuu wa Ihefu, Mecky Maxime amesema ana kazi kubwa ya kuimarisha safu ya ulinzi.
Maxime amesema kitendo cha kuruhusu mabao mawili kwa mchezo mmoja sio ishara nzuri hivyo anarudi katika uwanja wa mazoezi kushughulika na safu ya ulinzi ili makosa yasijirudie.
Kocha huyo amesema matokeo hayo yalikuwa bora kwao na walihitaji kushinda kwa idadi kubwa ya mabao.
“Bado tunahitaji ushindi zaidi wenye idadi kubwa ya mabao. Niwapongeze vijana walipambana japokuwa walipoteza umakini eneo la beki. Tunaenda kusahihisha makosa ili mechi ijayo na Geita Gold tufanye kweli,” amesema.
Kocha huyo ameongeza kuwa bado timu hiyo haipo katika sehemu nzuri na namna ya kuondoka nafasi za chini ni kuendelea kupambana kila mechi bila kujali nyumbani au ugenini ili kufikia malengo.
Ihefu haikuwa na mwanzo mzuri msimu huu hadi kuwafanya mabosi wa timu hiyo kufanya mabadiliko kwenye Benchi la Ufundi wakimacha Zuberi Katwila na kumpa majukumu Maxime ambaye ameyanza kibabe.