Wakati wakijiandaa kupapatuana na JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara baadae leo Alhamis (Februari 15), Mabosi na Benchi la Ufundi la Simba SC kwa pamoja wamesema bado wapo katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara licha ya kuachwa nyuma na watani zao, Young Africans kwa tofauti ya Pointi saba.
Simba SC yenye Pointi 33, imecheza michezo 14 na katika msimamo iko kwenye nafasi ya pili wakifuatiwa na Azam FC ambao pia wanalingana michezo wakiwa na Pointi 32 wakati mabingwa watetezi Young Africans wanaongoza wakiwa na Pointi 40.
Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhalk Benchikha, amesema licha ya timu yake kuzidiwa na watani zao, bado wapo kwenye mbio za ubingwa na hawana Presha yoyote kutokana na nafasi waliyopo.
“Ligi bado ina michezo mingi, huwezi kusema haiwezekani wakati bado kuna mechi za mzunguko wa pili, tutaendelea kupambana katika kila mchezo kuhakikisha tunavuna alama tatu,” amesema Benchikha.
Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema mechi ya leo inakwenda kumaliza michezo yao ya mzunguko wa kwanza na wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi utakaoendelea kuwapa morali kufikia malengo.
“Nina imani na wachezaji wangu, wamekuwa wananipa kile ambacho nawaagiza, tunaangalia michezo yetu zaidi, tunataka tushinde kila mchezo,” Benchikha amesema.
Kauli hiyo za Benchikha imepewa nguvu uongozi wa timu hiyo kupitia kwa Meneja wa Habari na Mawasiliano Ahmed Ally, ambaye amesema bado wanaendelea na mapambano ya kusaka ubingwa wa msimu huu 2023/24.
“Bado hatujatoka kwenye njia za ubingwa na hatuwezi kutoka, tumeanza kuona manufaa ya usajili wetu wa dirisha dogo kwa wachezaji wa nje, wanatupa kile tulichokuwa tunakihitaji kutoka kwao,” amesema Ahmed.
Amesema kwa wachezaji wao wa ndani waliowasajili hivi karibuni wanaendelea kuwapa muda na wanaamini wataisaidia timu hiyo kutokana na uwepo wao.
Ameongeza kuwa Simba SC hawana hofu yoyote kuelekea mechi dhidi ya JKT Tanzania ambayo itachezwa kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Meja Isamuhyo.
“Tunakwenda kufuata alama tatu, hatuiogopi JKT hata wakicheza kwao, tunataka kutimiza lengo letu msimu huu,” amesema Ahmed