Mshambuliaji Mohamed Salah ameonekana akiwa amerejea katika mazoezi ya Liverpool juzi Jumanne (Februari 13) huku nahodha huyo wa Misri akikaribia kurejea kutokana na jeraha la misuli ya paja.
Salah alipata jeraha hilo mapema katika Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ ambapo alikumbwa na utata aliporejea Liverpool kwa matibabu na alilazimika kukataa hadharani madai kwamba alikuwa ameliacha taifa lake.
Mpango ulikuwa Salah kurejea AFCON 2023 baadae katika kinyang’anyiro hicho lakini kuondolewa kwa mshangao kwa Misri kulimaanisha kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 angezingatia tu kurejea katika utimamu kamili.
Akiwa amekosa mechi nne zilizopita za Ligi Kuu ya England, Salah alirejea mazoezini juzi Jumanne (Februari 13) ili kujiunga na maandalizi ya safari ya keshokutwa Jumamosi (Februari 17) kuelekea Brentford.
Pia walionekana wakiwa mazoezini Mlinda Lango Alisson na beki Joe Gomez, ambaye alikosa mchezo wa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Burnley kutokana na ugonjwa, na beki wa kulia Conor Bradley, ambaye alipewa muda kuwa nje ya timu kwa sababu kibinafsi.
Thiago Alcantara amerejea uwanjani kutokana na jeraha jipya la misuli ambalo alilipata dakika ya tano katika mchezo waliofungwa mabao 3-1 na Arsenal ikiwa mechi yake ya kwanza tangu Aprili 2023 huku kiungo mwenzake Dominik Szoboszlai akiwa nje.
Liverpool wamekaa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu na kama watapata ushindi kwenye mchezo wa keshokutwa Jumamosi (Februari 17) utaongeza presha kwa wapinzani wake wa karibu Manchester City na Arsenal kwa ushindi dhidi ya Brentford.