Wachezaji wa Ivory Coast na Kocha wao wa muda Emerse Fae wamepewa fedha na nyumba za kifahari baada ya kutwaa Ubingwa wa Afrika ‘AFCON 2023’ kwa kuifunga Nigeria mabao 2-1 kwenye ardhi yao ya nyumbani Jumapili (Februari 11).
Kila mchezaji kwenye kikosi cha timu hiyo amepewa faranga za Ivory Coast Milioni 50 sawa na dola za Marekani 82,152 na nyumba za kifahari zenye thamani inayolingana na kiasi hicho cha fedha walizopewa.
Kocha Fae amepokea faranga Milioni 100 kwa kuiongoza timu hiyo kushinda ubingwa huo akichukua nafasi ya Jean-Louis Gasset katikati ya mashindano baada ya timu hiyo kufungwa mabao 4-0 na Guinea ya Ikweta.
“Mmeleta furaha kwa watu wa Ivory Coast, hongereni sana,” amesema Rais wa nchi hiyo, Alassane Ouattara.
Wachezaji pia walitunukiwa tuzo ya heshima kubwa kuliko zote kwenye taifa la Ivory Coast kwa mafanikio hayo.
Hilo ni taji la tatu kwa Ivory Coast kwenye michuano hiyo baada ya kuvuka hatua ya makundi kama mshindwa bora kutoka Kundi A.