Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeitaka Serikali kufanya tathimini ya utendaji kazi wa Ofisi ya Makatibu Tawala Mikoa katika kusimamia miradi yote ya maendeleo katika mikoa yao na kuchukua hatua stahiki kwa wote watakaobainika kutotekeleza wajibu wao kikamilifu.
Akisoma taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2023, Mwenyekiti wa LAAC, Halima Mdee amesema kamati imebaini kuwa Sekretarieti za mikoa zimeshindwa kutekeleza jukumu lake la usimamizi na ufuatiliaji wa miradi inayotekelezwa katika halmashauri zilizopo katika maeneo yao ya usimamizi.
Amesema, “Kukosekana kwa usimamizi wa mkoa katika halmashauri kumechangia kwa kiasi kikubwa kwa wakurugenzi wa halmashauri kutotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na miongozo ya Nchi na kuzorotesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.”
Mdee ameongeza kuwa, “Kamati imeazimia kuwa Sekretarieti za Mikoa zifanye ukaguzi wa miradi inayotekelezwa katika halmashauri zao na kuwasilisha taarifa zao Ofisi ya Rais-TAMISEMI kila robo ya mwaka.”
Aidha, Kamati pia imeazimia kuwa Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Sekretarieti za Mikoa kusimamia kikamilifu na kuhakikisha miradi yote iliyotekelezwa kwa kutumia njia ya force account ambayo haijakamilika inakamilika kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha ili iweze kutoa huduma iliyokusudiwa.