Afrika imekuwa ikishudia vituko vya baadhi ya Viongozi wao kwa namna wanavyoziendesha Serikali za Nchi, licha ya uwepo wa wachache ambao wamepata na wanaendelea kujitoa kwa ustawi wa bara la Afrika, wapo walioacha makovu makubwa kwa nchi zao akiwemo Mobutu Sese Seko.
Alizaliwa Octoba 14, 1930 huko Lisala na baadaye alipenda kuitwa Kuku Ngbendu wa Zabanga yaani “Shujaa mwenye enzi asiyeshindikana” ingawa alizaliwa na kupewa jina Joseph Desire Mobutu. Alipata kuwa raisi wa Congo zamani ikiitwa Zaire mwaka kati ya mwaka 1965 – 1997, baada ya kupinduliwa na Laurent Desiré Kabila.
Hakuishiwa vituko, alipambana kwelikweli kuhakikisha anatawala kwa njia alizoona yeye kuwa zinafaa na hapo wakati mwingine alijikuta akifanya vituko ambavyo leo hii ningependa uvifahamu japo kwa uchache juu ya Kiongozi huyu aliyekuwa mtu wa matukio ambayo yameacha alama si tu kwa DRC bali Africa kwa ujumla.
Kila alipofanya ziara zake kwenda nje ya nchi aliondoka na wakuu wa majeshi wote pamoja na funguo za maghala yote ya silaha akihofia kupinduliwa na wakuu wake wa majeshi. Yaani alihakikisha hakuna funguo za magala ya silaha zinabaki nyuma wala wanajeshi wa vyeo vya juu.
Miaka ya 1970/1971 Mobutu alitangaza kile alichoita “kempeni ya utamaduni wa Kiafrika”. Alitoa amri kwa raia wote wenye majina ya kikristo kuyaacha na kutumia majina yanye asili ya Afrika, Haitoshi alibadilisha jina la Kongo kuwa Zaire. Alipiga marufuku Suti za Ulaya, mwenyewe alianza kuvaa suti zilizoiga mfano wa Mao-Tse-Tung.
Mpaka kufikia Mwaka 1984 alikuwa ni moja ya Rais wenye ukwasi wa maana, alihifadhi karibu dola bilioni 4 za Marekani. Yeye alikuwa na uchumi imara kuliko nchi anayoiongoza. Watoto wake walipelekwa shuleni jijini Paris Ufaransa Kila Siku na jioni kurudi nyumbani Kinshasa kwa ndege ya Concorde. Lakini kwa sasa binti yake mdogo aitwaye NGAWALI ni mhudumu wa mgahawa huko Paris.
Mobutu alikuwa mpenda soka, inaarifiwa kuwa aliwahi aliita Wachawi na Waganga wote jijini Kinshasa pale Taifa hilo lilipopata nafasi ya kushiriki kombe la Dunia Ujerumani mwaka 1974. Akawakodia ndege kwenda kuwaganga wachezaji. Walitua na madawa yao na kufukiza usiku kucha na siku ya mechi ya kwanza ilipofika dhidi ya Yugoslavia, Zaire walitandikwa 9-0.
Aliwahi pia kutunga sheria iliyotaka vituo vyote vya Runinga kuonesha picha yake akishuka mawinguni kila siku jioni kabla ya Taarifa ya Habari kuanza. Haitoshi akaongeza na kipengele kuwa wanapaswa kutaja jina lake tu sio mtu mwingine.
Akiwa anafurahia maisha na wanawe Kongulu Mobutu, Nzanga Mobutu, Giala Mobutu, Yakpwa Mobutu, Manda Mobutu, Nyiwa Mobutu na Konga Mobutu kwa kula Kuku kwa mrija huku uchumi wa Zaire ukiyumba, Mobutu alijenga uwanja wa ndege wenye uwezo wa kutua ndege kubwa kama Concorde kwenye hekalu lake kijijini kwao Gbadolite.
Kabla Mobutu hajafariki, alitaka mwili wake uchomwe moto na majivu ya mwili wake yasambazwe kwenye ardhi ya nchi aliyozaliwa na kuiongoza kama mfalme.
Kulikuwa na migomo ya Wanafunzi wa Vyuo Vikuu miaka ya 1969, walipinga nguvu iliyotumika. Wanafunzi kadhaa walikufa na aliamuru wanafunzi 2000 wengine wakamatwe na waingizwe katika jeshi, ili wajifunze nidhamu. Amri hiyo ilitekelezwa na wanafunzi hao walilitumikia jeshi.
Mobutu akiwa msaidizi wa Lumumba, akishirikiana na Joseph Kasavubu katika uasi dhidi ya Waziri Mkuu wa kwanza, Patrice Lumumba aliyepinduliwa Septemba, 1960. Ilipofika 16 Mei 1997 jeshi la Rais Kabila (Baba wa aliyekuwa Rais Joseph) walitwaa uwanja wa ndege wa Lubumbashi na Mobutu alikimbilia Togo na kuomba hifadhi Ufaransa lakini Ufaransa ilikataa, hivyo alienda kuishi Morocco, ambapo aliishi kifahari licha ya kuwa mgonjwa.
Inasemekana Mobutu Sese Seko alifariki Septemba 7, 1997 huko Morroco akiwa na umri wa miaka 66, lakini haikutangazwa kwani habari zake zilizuiwa na cha kusikitisha alizikwa na watu wanne tu huko Morroco. Ulikuwa mwisho mbaya kwa Kiongozi mkubwa aliyemiliki akaunti za mabilioni huko uswisi. Baadae familia yake ilikwenda kufanya mazishi upya.