Kocha wa Makipa wa Simba SC, Daniel Cadena amesema ushindi walioupata juzi Alhamis (Februari 15) dhidi ya JKT Tanzania, umewaongezea ari ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Simba SC ilibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuendelea kubaki nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 36 ikiwa nyuma kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya vinara Young Africans.
Akizungumza jijini Dar es salaam kocha huyo raia wa Hispania, amesema wachezaji wao walijituma na kufuata maelekezo waliyowapa kwa sehemu kubwa ndiyo sababu wakavuna pointi hizo tatu ambazo zimefufua matumaini ya kukaa kileleni na kurudisha taji hilo msimu huu 2023/24.
“Ulikuwa mchezo mgumu lakini kitu cha kufurahisha pamoja na ubovu wa uwanja, lakini vijana walijituma kwa kufuata kile ambacho tumewaelekeza lakini kipa wetu Ayoub Lakred alikuwa kwenye kiwango bora sana kutokana na kazi kubwa aliyoifanya anastahili pongezi,” amesema Cadena.
Aidha, kocha huyo amesema sababu ya kucheza bila Mshambuliaji halisi ni kutokana na kufanya mzunguuko wa kikosi na hiyo imetokana na kucheza mechi nyingi kwa kipindi kifupi hivyo wamewapumzisha wachezaji kwa ajili ya mechi zinazofuata.