Klabu ya Tottenham Hotspur imeanza kupata wasiwasi wa kumpoteza kocha wao Ange Postecoglou, anayehusishwa na mpango wa kuwaniwa na Klabu ya Liverpool mwishoni mwa msimu huu.
Tayari Kocha Mkuu wa Liverpool, Jurgen Klopp ametangaza kuachana na miamba hiyo ya Anfield utakapofika mwishoni mwa msimu huu, kitu ambacho kitafanya mabosi hao wa Merseyside kuingia sokoni kusaka kocha mpya.
Liverpool ilipambania mataji manne msimu huu, huku ikifahamika wazi itarejea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao, hivyo kuondoka kwa Klopp kunawapa changamoto kubwa mabosi wa timu hiyo katika kutafuta kocha mwingine ambaye atakuwa na uwezo wa kuendelea walipoishia.
Tangu Klopp alipotangaza ataachana na timu hiyo mwisho wa msimu, majina kadhaa ya makocha yamehusishwa na miamba hiyo ya Anfield, akiwamo wa Bayer Leverkusen, Xabi Alonso.
Mhispaniola huyo, Alonso, ambaye ni kiungo wa zamani wa Liverpool, bado hajapoteza mchezo wowote kwenye kikosi cha Leverkusen msimu huu, huku timu yake ikiweka pengo la Pointi tano kwenye kilele cha msimamo wa Bundesliga mbele ya Bayern Munich.
Ukimweka kando Alonso, kocha mwingine ambaye ameripotiwa kuwapo kwenye rada za Liverpool ni mkali huyo wa Spurs, Postecoglou, ambaye amekuwa akifanya mambo makubwa kwenye kikosi hicho cha London tangu alipotua akitokea Celtic.
Makali ya Postecoglou huko Spurs ndiyo yanayowapa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo na kuamini wanaweza kumpoteza kocha wao endapo kama Liverpool watageukia huduma yake.