Kocha kutoka nchini Ureno Jose Mourinho anaamini Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City ndio washindani wakuu wa taji la Ligi ya mabingwa Barani Ulaya msimu huu, lakini anatarajia Real Madrid itatoa Ushindani mkubwa kwenye mbio za kuwania Ubingwa huo.
Man City ilitwaa Ubingwa wa Michuano hiyo msimu uliopita, na kushinda mataji matatu na kumaliza msimu bora kabisa katika historia ya klabu hiyo.
Kikosi cha Pep Guardiola kinapigiwa upatu kutwaa tena Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, huku pia wakipania kuwa timu ya kwanza kushinda Ligi Kuu ya England kwa miaka minne mfululizo.
Wakati akifanya mahojiano na Rio Ferdinand, Mourinho aliulizwa utabiri wa washindi wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya na Ligi Kuu ya England msimu huu.
“Ligi ya Mabingwa Ulaya, ningesema City au Real Madrid. Ikiwa klabu nje ya hizo mbili itashinda, kwangu, itakuwa mshangao mkubwa,” amesema.
“Ningependa Real Madrid kushinda tena kwa klabu na kwa Carlo Ancelotti. Sijui, Bayern Munich wanaweza kufanya hivyo na Paris Saint-Germain.
“Nikiangalia uwezo, nadhani City/ Liverpool kwa Ligi Kuu, City/ Real kwa Ligi ya Mabingwa Ulaya.”
Wakati Mourinho hakushinda Ligi ya Mabingwa Ulaya katika misimu yake mitatu akiwa na Madrid, nafasi yake ilichukuliwa na Ancelotti, ambaye alishinda Ligi ya Mabingwa katika msimu wake wa kwanza pale Santiago Bernabeu na sasa anawinda Kombe lake la tano la Ulaya kama kocha.