Kwa mujibu wa taarifa kutoka Daily Mail, FC Barcelona sasa imedhamiria kumwajiri Kocha wa Brighton, Roberto De Zerbi msimu ujao baada ya Rais wa timu hiyo kuomba ripoti yake.

De Zerbi ambaye ana mkataba wa kuitumikia Brighton hadi mwaka 2026, ameonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuvutia vigogo wengi.

Barca inaamini De Zerbi anafaa kuchukua nafasi ya Xavi, ambaye ametangaza ataondoka mwisho wa msimu huu.

Kwa mujibu wa ripoti kutoka Diario Sport imethibitishwa Rais wa Barca, Joan Laporta ameomba kupewa wasifu kamili wa De Zerbi kabla hajaanza naye mazungumzo ya kumshawishi achukue mikoba ya Xavi.

Wakala wa kocha huyu hivi karibuni aliripotiwa kuwasili Hispania hali iliyozidisha tetesi kuna uwezekano kukawa na mazungumzo yanayoendelea.

Laporta anasaidiana na Mkurugenzi wa masuala ya mpira wa miguu wa timu hiyo, Deco na mpango wao ni kuhakikisha kocha mpya anaajiriwa mapema kwa ajili ya kwenda na timu kwenye maandalizi ya msimu ujao.

De Zerbi aliiwezesha Brighton kufuzu michuano ya Ulaya kwa msimu uliopita na anaonekana huenda akarudia tena hilo msimu huu.

Inaelezwa Brighton imeshajiandaa na maisha bila ya kocha huyu kwa sababu imetengeneza falsafa maalumu ambayo kila kocha anayekuja atatakiwa kuifuata.

GGML yazindua mpango wa mafunzo kazini
Kiduku: Maneno ya nini Mwakinyo aje ulingoni