Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema ushindi dhidi ya KMC FC ni iashiria tosha kwamba wamedhamiria kutetea taji lao la Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya tatu mfululizo.
Ushindi huo wa mabao 3-0, umeifanya miamba hiyo kuzidi kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi ikifikisha Pointi 43 katika michezo 16 huku wakifunga mabao 39.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema anafurahishwa na juhudi zinazofanywa na wachezaji wake ambazo zimekuwa zikiwapa matokeo yanayowaweka karibu na lengo lao kuu ambalo ni ubingwa.
“Pamoja na ushindi tulioupata lakini nimefurahi namna timu ilivyocheza, tulikuwa kwenye ubora tuliokuwa nao kabla ya mapumziko ya ‘AFCON 2023’, kila mchezaji alicheza kwa kujitoa kuipigania nembo ya Young Africans, hiki ndicho nataka kukiona katika kila mechi na ushindi huu unatupa nguvu ya kutimiza kusudio letu la kutetea taji,” amesema Gamondi.
Kocha huyo pia ameigusia safu yake ya ushambuliaji ambayo ilipoteza nafasi nyingi za wazi hasa kipindi cha kwanza hasa mshambuliaji Clement Mzize akisema, siyo kitu ambacho alitegemea kutokana na mbinu alizowapa lakini ataenda kufanya maboresho kabla ya mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya CR Belouizdad.
Naye Kocha Mkuu wa KMC, Abdulhamid Moallin amekiri kwamba walikutana na timu bora iliyowazidi kila kitu na ndio sababu ya kupoteza mchezo huo.
Amesema kasi waliyoanza nayo wapinzani wao Young Africans na kuruhusu bao la mapema viliwachanganya wachezaji wake na kujikuta wakishindwa kufuata kile ambacho amewaelekeza na kujikuta wanapoteza mchezo huo.