Kwa mujibu wa tovuti ya Footmercato, Rais wa Real Madrid, Florentino Perez amewaambia wachezaji wa timu hiyo kwamba mshambuliaji wa PSG, Kylian Mbappe atajiunga na kikosi hicho katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mbappe tayari ameshawaambia mabosi wa PSG kwamba ataondoka kama mchezaji huru katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Awali, dili la Mbappe kutua kwa wababe hawa lilidaiwa kusuasua kutokana na kutofikiwa muafaka kwenye masuala ya maslahi binafsi lakini kwa sasa kila kitu kimekaa sawa.
Kwa mujibu wa ripoti ni kuwa staa huyu tayari ameshaandaliwa hadi jezi ambayo atakuwa anaivaa ambayo ni namba 10.
Dili la Mbappe linadaiwa kuigharimu Madrid zaidi ya Pauni 150 milioni kwenye masuala ya bonasi ya usajili na mshahara wake unakadiriwa kufikia Pauni 50 milioni kwa msimu.
Kiungo wa Madrid, Aurelien Tchouameni aliweka picha ya popcorn kwenye ukurasa wake wa Twitter kama fumbo la kumsubiri kwa hamu.