Mbunge wa Makete, Festo Sanga amependekeza njia za kupata fedha za kuandaa Fainali za za Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON’ zitakazofanyika mwaka 2027.
Sanga amesema kuwa ana imani Fainali hizo zitaweka historia na mfano kwa nchi nyingine.
“Unajua mwaka 2027, AFCON itafanyika Tanzania, Kenya na Uganda, sasa kunahitajika fedha nyingi kwa ajil ya maandalizi, ‘amesema.
Amepongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu kubwa kuhakikisha michuano hiyo inafanyika.
“Kitendo cha kupata nafasi ya kuandaa michuano hiyo, kikubwa inabidi tuwapongeze Marais wetu wa Tanzania, Kenya na Uganda, wamefanya kazi kubwa,’ amesema.
Sanga amesema kutokana na hali hiyo, anapendekeza serikali ni vyema ikashirikiana na wadau kupata fedha za kufanikisha jambo hilo.
“Nimekaaa na kuona nitoe maoni au ushauri wangu kwa kuwa kuna changamoto ya ufinyu wa bajeti katika Wizara ya Michezo, vyema serikali iamue kwa nia ya dhati kutumia fedha zote zinazotokana na gawio za mashirika ya umma ya serikali zaidi ya asilimia 66, kupeleka huko,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali inaweza ikatumia fedha za CSR (Corparate Social Responsibility) zinazotakiwa kutolewa na kampuni kubwa zinazofanya kazi nchini.
Sanga ametoa mfano wa kampuni zinazojenga reli ya kisasa maarufu ‘SGR, bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere.
Amefafanua kuwa kampuni nyingine ni zile zinazoshughulika na kuchimba madini sehemu mbalimbali hapa nchini.
“Nashauri fedha hizo, zikiwekwa kwa miaka mitatu mfululizo, zielekezwe katika mfuko maalum wa michezo hususan maandalizi ya ‘AFCON 2027’” amesema Mbunge huyo.
Sanga amesema kwa kufanya hivyo, kutatuhakikisha kupatikana fedha za kutosha zitakazosaidia kujenga viwanja vya kucheza mashindano hayo na kufanyika mazoezi.
“Kupitia fedha hizo, nina uhakika tutaweza kupata Viwanja vya kufanyla mazoezi kwa timu zote zitakazo kuja hapa nchini na nmiundombinu ya michezo na kambi za timu zetu,”amesema.