Mlinda Lango wa KMC FC, Wilbol Maseke amewaomba radhi Mashabiki wa Soka nchini Tanzania kwa kitendo chake cha kumrushia ngumi mchezaji mwenzake Ibrahim Mao kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Young Africans uliochezwa uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro juzi Jumamosi (Februari 17).

Tukio hilo lilitokea baada ya KMC FC kufungwa bao la kwanza dakika za mapema kutokana na makosa ya Maseke na kumfanya aendelee kufanya makosa mengi ndipo Ibrahim Mao akaenda kumshauri atulie na kusababisha ugomvi huo.

Dakika ya 46, KMC ilifanya mabadiliko ya Mlinda Lango kwa kumtoa Maseke na nafasi yake ikachukuliwa na Denis Richard.

Maseke ametumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kuomba radhi kwa kile kilichotokea kuwa sio cha kimichezo.

“Poleni mashabiki zangu na wanaopenda kazi ninayofanya nikiwa uwanjani, niombe radhi kwa kitendo kilichojitokeza mimi kugombana na mwenzangu.”

“Haikuwa kusudio langu, pia baada ya hapo ukweli ni kwamba sikuendelea na ugomvi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo bali yale ni maamuzi ya mwalimu kunitoa nimeheshimu hilo,” ameandika Maseke.

Maseke ameongeza kuwa ana mengi ya kusema ambayo huwa yanaendelea nje ya uwanja ambayo yalisababisha kuharibu saikolojia yake lakini akaomba wamsamehe kwa kilichotokea.

Mmoja afariki kwa ajali ya Bajaji, Basi dogo Moro
Pascal Wawa aishtua Simba SC Ivory Coast