Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila, ameitaka Kampuni Group Six lnternational, kukamilisha ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni (KMC), kabla ya Machi 30, mwaka huu.
Chalamila ametoa agizo hilo baada ya kukagua ujenzi wa uwanja huo uliopo Mwenge jijini Dar es salaam.
Amesema kasi ya utekelezaji wa mradi huo hairidhishi, fedha za ujenzi wa uwanja zilizotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zinapaswa kufanya kazi kikamilifu na kwa wakati.
“Kazi ya ujenzi ifanyike usiku na mchana na uwanja ukamilike kabla ya Machi 30, mwaka huu.” amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amesema endapo mradi huo hautakamilika kwa wakati, ataagiza mkandarasi asipewe kazi nyingine.
Pia, Chalamila amesema mkandarasi anapaswa kuboresha uwanja katika baadhi ya maeneo ikiwemo kuwekwa jukwaa la Watu Mashuhuri (VIP).
Mkuu wa Wilaya Kinondoni, Saad Mtambule, amesema uwanja huo uko katika hatua za ukamilishwaji pamoja na miradi ya kimkakati ya stendi ya kisasa, mradi wa zaidi ya sh. bilioni 12 uliopo Tandale.
Amesema baada ya kukamilika miradi hiyo, Kinondoni itatengeneza ajira, kuunganisha watu pamoja kuongeza mapato ya halmashauri.
“Miradi hii ikikamilika itaingiza mapato kwa halmashauri yetu ya Kinondoni, uwanja unatarajia kuingiza zaidi ya sh. milioni 400, stendi itangiza sh. milioni 800 kila mwaka”, amesema.
Meya wa Kinondoni, Songolo Mnyonge, amesema mkandarasi anapaswa kuongeza kasi ya ujenzi na kukamilisha mradi kwa wakati.