Wakati kikosi cha Simba SC kikiwa safarini kuelekea nchini Ivory Coast kwa ajili ya mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi B Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Asec Mimosas, Kocha Mkuu wa Miamba hiyo ya Kariakoo Abdelhak Benchikha amekiri kufurahishwa na hatua ya kuahirishwa kwa mechi ya Mtibwa, ambayo imempa nafasi ya kuwaandaa wachezaji wake, baada ya kucheza bila kupumzika kwa siku 15.

Simba SC imeondoka mapema Alfajiri leo Jumanne (Februari 20) ikiwa na kikosi cha wachezaji 23 kuelekea Addis Ababa nchini Ethiopia, ambako watakaa kwa saa tatu kabla ya kuunganisha ndege kuelekea jijini Abidjan tayari kwa mchezo huo utakayochezwa Jumamosi (Februari 24) katika Uwanja wa Felix Houphouet Boigny nchini humo.

Kocha Benchikha amesema aliushawishi Uongozi wa Simba SC kuliandikia barua Shirikisho la Soka nchini Tanzania na Bodi ya Ligi ‘TPLB’ ili mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uahirishwe, kutokana na hitaji la kiufundi, ambalo lilipaswa kufanyiwa kazi kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ivory Coast.

“Ni mimi ndiye niliyeomba mechi hii iahirishwe ili kupata nafasi kuwa na vijana wangu kwa ajili ya mazoezi ya jumla, kwani siku zote 15 tulikuwa tunafanya mazoezi kwa ajili ya mechi zilizokuwa zinafululiza, kwa hiyo lilikuwa ni takwa la kiufundi. Tunakwenda kukutana na mpinzani mgumu, hivyo lazima upate muda wa kuwaandaa wachezaji.

“Pili ni hatari ya kupata majeraha, katika mechi dhidi ya JKT Tanzania tulipata majeruhi watatu ambao ni Clatous Chama, Sadio Kanoute na Kibu Denis na hiyo ni kutokana na tatizo la ubovu wa uwanja,” amesema Benchika kabla ya kuondoka nchini.

Simba SC itateremka dimbani ikiwa kwenye nafasi ya pili ya msimamo wa Kundi B, ikiwa na pointi nne, huku Asec Mimosas ikiwa imeshafuzu na pointi zake 10, hivyo inacheza kwa kukamilisha ratiba.

Katika hatua nyingine, Kocha wa makipa wa Simba SC, Daniel Cadena, ameweka wazi juu ya mabadiliko na kutokuwa na kipa namba moja, kuwa ni kutokana na waliokuwapo ndani ya kikosi cha timu hiyo wameonyesha uwezo mkubwa kila anayepewa nafasi.

Cadena amesema kulingana na ubora wa makipa walionao wamekuwa na wakati mgumu wa kuweza kupata kipa namba moja na kila mmoja amekuwa akipewa nafasi ya kucheza katika mechi tofauti.

Amesema anajivunia kuona makipa wake wanakuwa imara zaidi na kusaidia timu kupata matokeo chanya akiwamo Ayoub, ambaye mechi ya Ligi Kuu iliyopita aliweza kuzuia mashuti mengi kutoka kwa wapinzani wao, JKT Tanzania.

“Ninajivunia kuwa na makipa wazuri na wenye uwezo mkubwa, ukiangalia kiwango cha Aishi Manula, Hussein Abell, Ally Salim hata Lakred wote wapo vizuri hata mmoja wapo asipokuwapo ndani ya timu kwa changamoto yoyote hatuna presha ya nani kukaa golini,” amesema kocha huyo.

Gamondi: Tunatakiwa kuifunga CR Belouizdad
REB yatarajia matokeo kuwatumikia Wananchi