Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi, amesema ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele katika hatua ya Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ni lazima wapate ushindi wa mabao mengi dhidi ya wapinzani wao, CR Belouizdad ya Algeria utakaochezwa Jumamosi (Februari 24) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Gamondi amesema baada ya matokeo ya sululu kati ya CR Belouizad na Al Ahly ljumaa iliyopita nchini Algeria, Kundi lao limekuwa gumu na kitu pekee kitakachofanya kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kwenda Robo Fainali ni ushindi wa mabao mengi, kabla ya kubakisha mechi moja dhidi ya Al Ahly Ugenini.
Katika Kundi hilo, Young Africans inashika nafasi ya tatu ikiwa na alama tano sawa na CR Belouizdad ambaye ipo nafasi ya pili, Medeama FC ipo nafasi ya nne kwa kukusanya pointi nne na Al Ahly inaongoza kundi hilo ikiwa na alama sita.
Gamondi amesema wanafanya maandalizi mazuri kwa ajili ya kutafuta ushindi katika mchezo huo dhidi ya CR Belouizdad ili kujiweka katika nafasi nzuri katika msimamo wa kundi hilo.
Amesema wako kwenye kundi gumu ambalo kila timu ina nafasi ya kwenda hatua ya Robo Fainali hali ambayo wanatakiwa kupambana na kuumiza kichwa ili kusaka ushindi kwa mechi hiyo ya nyumbani.
“Hakika kila timu inaweza kwenda Robo Fainali kulingana na kundi lilivyo, tunasahihisha makosa yetu, tumefanikiwa kufanya vizuri kwenye safu ya ulinzi, lakini hata kushambulia kwa sababU ya kila mechi tumefanikiwa kufunga bao,” amesema Gamondi.
Amesema mechi dhidi ya CR Belouizdad haitakuwa rahisi kwa sababu ya ugumu wa Kundi hilo, lakini pia baada ya kuwaona wapinzani wake katika mechi na Al Ahly.
“Nimefanikiwa kuangalia mechi yao na Al Ahly, nimeona ubora wao walicheza vizuri na tumeanzia mechi hiyo kufanya maandalizi yetu kuelekea mchezo wetu ujao,” amesema kocha huyo raia wa Argentina.