Mashabiki wa soka na gwiji wa Arsenal, lan Wright wamemtaka kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate kuhakikisha anamjumuisha kiungo wa Manchester United, Kobbie Mainoo kwenye kikosi kijacho cha Three Lions.
Kiungo huyo kinda wa Man United, Mainoo mwenye umri wa miaka 18, amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kocha Erik ten Hag tangu alipoanza kutumika Desemba mwaka jana.
Ameanzishwa katika mechi zote tisa za mwisho ilizocheza za Man City kwenye Ligi Kuu England na ameonyesha ubora mkubwa ikiwamo kwenye mchezo wa juzi Jumapili wa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Luton.
Mainoo amecheza mechi 17 tu kwenye kikosi cha wakubwa cha Man United, amefunga mabao mawili, likiwamo moja matata kabisa la ushindi kwenye Ligi Kuu England dhidi ya Wolves.
Lakini, tayari kuna watu wanaamini ameshaiva kwa ajili ya kuitwa kuichezea England kwenye mechi zao mbili zijazo dhidi ya Brazil na Ubelgiji.
Gwiji wa Arsenal, Wright aliandika kwenye Twitter: “Kobbie Mainoo anapaswa kuwapo kwenye kikosi kijacho cha England. Ule ukomavu alionyesha kwenye mechi yenye utata sijapata kuona kwa mchezaji wa England kwa muda mrefu sana. Ananivutia kila wakati ninapomtazama.”
Na mashabiki kibao wamesapoti kauli ya mkali huyo wa Arsenal, ambapo mmoja aliandika: “Mainoo hajaitwa tu kwenye kikosi cha England, anapaswa kuwamo kwenye kikosi cha wachezaji 11 wa kwanza.”
Mwingine aliongeza: “Kobbie Mainoo anapaswa kuanza kwenye Michuano ya Euro 2024. Ni aina ya mchezaji ambaye England imekuwa ikimkosa kwenye michuano mikubwa.”
Shabiki wa tatu alisema: “Mainoo ni mchezaji siriazi. Ameonyesha anastahili kuwa sehemu ya kikosi cha England.”